NGUVU NA FAIDA ZA MSAMAHA



                             NGUVU NA FAIDA ZA MSAMAHA
TAREHE 15/6/2018.
SIKU YA TANO
Mwl. Lameck Kijalo

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe sana wana wa Mungu.
Baada ya kujifunza mambo mengi kuhusu "MSAMAHA" kutoka kwa Watumishi wa Mungu .
Karibu tena katika mwendelezo wa somo letu katika semina hii.
Na hakika utazidi kujifunza mengi zaidi.
VIPENGELE TUTAKAVYOENDA KUVIANGALIA  
Vipengele hivyo yamkini vimeisha fundishwa au bado lakini ni wakati wako mzuri wa kurudia au kujifunza upya. Vipengele hivyo ni:
1.Je neno msamaha au kitendo cha msamaha kilianzaje?
2.Je Sifa za mtoa msamaha ni zipi?
3.Je sifa za Muomba msamaha  ni zipi?
4.Njia unazoweza kutumia kuomba msamaha ni zipi?

1.CHANZO CHA MSAMAHA.
Msamaha ni neno linalomaanisha "Kuachilia"
Luka 6:37 ".achilieni nanyi mtaachiliwa."
Sasa jiulize msamaha ulianzaje!?
Ø  Msamaha ulianza pale dhambi au makosa yalipoanza. Maana bila dhambi au makosa msamaha usinge kuwepo, hivyo msamaha upo  maalumu Kabisa kwa ajili ya watenda dhambi au wafanya makosa.
Hivyo tambua kuwa penye dhambi au makosa hapo ndipo penye msamaha. Na huo msamaha huwepo hapo maalumu kwa anayetaka kuuomba ikiwa amekosea au ametenda dhambi, na pia upo kwa ajili ya mtu anayetaka kuutoa ikiwa ametendewa mabaya na Mtu fulani.
Ø  Umeona nasema msamaha upo mahali penye watu wanaohitaji kuomba msamaha au wanaotaka kutoa msamaha. Hii ina maana MSAMAHA ni Roho.  Na hii Roho ni Roho ya Mungu Kabisa kwani asili ya Msamaha ni Mungu mwenyewe.
Tambua tangu awali Mungu alifanya jitihada za kumsamehe Mwanadamu baada ya kutenda dhambi. Hivyo ukikuta mtu ameomba msamaha wa kweli ujue ndani yake ameingiliwa na Roho ya Msamaha ya Mungu, Na ukikuta mtu ametoa msamaha wa kweli ujue ameingiliwa na Roho wa Mungu wa Msamaha.
Ø  Roho ya kutokuomba msamaha au kutotoa msamaha ni roho ya Shetani. Na hii roho ilianzia mbinguni. Shetani alipoasi mbinguni hakutaka kuomba msamaha zaidi aliendelea kuutetea Uovu wake kwa kufanya vita na Mungu. Hatimaye Shetani alitupwa duniani, ambapo hana fulsa tena ya kuomba msamaha na kama alivyofanya kule mbinguni ndivyo anavyofanya duniani kwa wanadamu. Shetani amewafanya watu kutenda dhambi au makosa na kuwafanya wawe na mioyo ya kutoomba msamaha na kutotoa msamaha!
Tambua kuwa asiyesamehe hawezi kuomba msamaha, na asiyeomba msamaha hawezi kusamehe. Hapa ndipo penye roho wa Shetani kutenda kazi.
Kama ambavyo hatma ya Shetani kutoomba msamaha na kutokuwa na fulsa tena ya kutoweza kuomba msamaha baada ya kutupwa duniani, ndivyo ilivyo kwa mwanadamu ambapo hatma ya kutoomba msamaha au kutotoa msamaha ipo baada ya kifo chake. Mtu akifa hana fulsa ya kuomba wala kutoa msamaha.
Tambua kuwa roho wa Shetani hujigeuza geuza na wakati fulani kuonekana kama ni Roho wa Mungu, 2Wakorintho 11: 14 "Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hijigeuza  awe mfano wa malaika wa nuru"  na hapa ndipo penye kutolewa msamaha wa uongo, na kuomba msamaha wa uongo.
Hii ina maana gani? Hii ina maana wapo watu ambao hujifanya wanakusamehe huku moyoni mwao wamejenga kisasi, na kwa kuwa mtu ataona amesamehewa atajenga ukaribu na mtu huyo, lakini mtu huyo anaweza kuja kumfanyia kitu kibaya zaidi ya kile alichofanyiwa, halafu naye ataomba msamaha kama ulivyomuomba msamaha."Fikiria sana hili"
Lakini wapo watu huomba msamaha wa uongo, na wakisamehewa tu basi hufanya kosa kubwa zaidi ya lile! "Kuwa mwangalifu"
Si kila anayesamehe amesamehe kweli, na si kila anayeomba msamaha huwa anamaanisha.
Kusamehe ni kinyume cha kuhukumu. Mtu asipokusamehe maana yake ameamua kukuhukumu. Penye msamaha pana kuwekwa Huru, Na mahali pasipokuwepo msamaha pana hukumu.
Mathayo 7:1 "Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi."
Hii ina maana usipo samehe kamwe nawe huwezi kusamehewa. Hii ina maana gani? Kile unachomtendea mwenzio ndicho utakacho tendewa.




SIFA ZA MTOA MSAMAHA

Hapa naongelea mtoa msamaha wa kweli, yaani anaye maanisha.
Mtoa msamaha wa kumaanisha huwa na sifa zifuatazo:
A. Huwa ni mtu mwenye uvumilivu.
B. Huwa ni mtu mwenye Huruma.
C. Huwa ni mtu mwenye Upendo.
D. Huwa ni mtu mwenye kujua umuhimu wa kusamehe.
E. Huwa ni mtu anayemjua Mungu ambaye ndiye chanzo cha msamaha.
Ø  Mtu mwenye sifa hizo hapo juu ni mtu anayejua hasa nini maana ya kusamehe. Na ili ujue amekusamehe hata kabla ya kumuomba msamaha basi:-
A. Atakuwa anakusalimia.
B. Ukiwa na tatizo atakusaidia.
C. Atakuwa mchangamfu kwako.
D. Hawezi kukusema vibaya kwa watu.
E. Kama ni deni hawezi kukudai dai.
Hizi ni dalili za mtu ambaye anaweza kukusamehe au amekusamehe hata kabla hujamuomba msamaha.

3. SIFA ZA MUOMBA MSAMAHA
Mtua ambaye ametenda dhambi au amefanya makosa ili aonekana anaomba msamaha kwa kumaanisha ni sharti awe na sifa zifuatazo:-
A. Ajue umuhimu wa kuomba msamaha.
B. Ajue njia sahihi za kuomba msamaha.
C. Ajue namna ya kumfanya asirudie kutenda dhambi au kurudia makosa.
D. Ajue umuhimu wa kuwa na Roho Mtakatifu.

Tumeona asilimia kubwa ya watu ambao wametenda dhambi au kufanya makosa huja kuomba msamaha wakati hali zao za kimaisha zimekuwa mbaya, kwa mfano kupatwa na magonjwa, kufirisika kiuchumi, kufukuzwa kazi, n.k.
Sasa hapa hawa watu wanaosukumwa na matatizo au shida zao kuja kuwaomba msamaha walio wakosea huwa ni vigumu kujua wana maanisha au hawamaanishi, kwani unaweza kuwasamehe lakini baada ya hali yao kuwa nzuri wanarudia Tabia zao zile zile, hivyo Wewe mtoa msamaha kwa watu kama Hawa, ishi nao kwa makini sana na muachie Mungu maisha yake huyo mtu
Ni vyema mtu ukaomba msamaha ukiwa katika hali yako ile ile uliyomtendea mtu kosa, au ukiwa kwenye hali nzuri, kwani msamaha wako utakuwa na uzito na utaonekana umejinyenyekeza sana tofauti na ukisubiri upatwe na mabaya kwani hapo utaonekana umenyenyekezwa na matatizo. Mara nyingi hiari ya mtu iko kwenye mafanikio yake, kama yuko kwenye matatizo mara nyingi huwa si hiari yake kufanya maamuzi.

4 .NJIA SAHIHI MBALIMBALI ZITUMIKAZO KUOMBA MSAMAHA
Kuna njia nyingi ambazo mtu abayejua kuwa amekosea au ametenda dhambi anaweza kuzitumia anapoamua kutaka kuomba msamaha...
Njia hizo ni:-
        I.            Tambua kuwa umemkosea Mungu na Mwanadamu, Hivyo anza kuomba msamaha kwa Mungu kwanza kisha nenda kwa mtu uliyemkosea.

     II.            Kujutia makosa na kulia mbele ya uliyemkosea ambaye ni Mungu na mwanadamu. Machozi hugusa na huonyesha uchungu wa mtu.

  III.            Yamkini si rahisi Wewe mwenyewe kuomba msamaha hivyo hauna budi kuwaomba watu au mtu kukuombea msamaha kwa uliyemkosea.

  IV.            Kumshawishi kwanza mtu yule uliyemtendea kosa. Kwa mfano Kumnunulia Zawadi, kumsaidia kitu, Kujipendekeza kwake, ili iwe rahisi kumuomba msamaha.

     V.            Kumrudia rudia mtu yule unayemuomba msamaha ili akusamehe ikiwa utaona hajakusamehe, huwezi jua kama anakupima kama ulimaanisha kuja kwake kumuomba msamaha?

  VI.            Kusujudu au kupiga magoti mbele ya yule uliye mkosea. Hii pia huonyesha kujutia makosa na unyenyekevu  kwa uliyemkosea

VII.             Kumuandikia barua au ujumbe wa kumuomba msamaha uliye mkosea ikiwa itaonekana ni vigumu kuonana naye. Japo msamaha wa ana kwa ana unafaa zaidi.
Tambua kuwa unaweza tumia njia zaidi ya moja wakati wa kuomba msamaha ili kutimiza kusudi lako la kusamehewa. Tambua kuwa unaweza kuja kuomba msamaha halafu ukashindwa kusamehewa kwa sababu ya kutumia njia mbaya ya uombaji msamaha, mfano kauli au maneno yako yanaweza kukusaidia usamahewe au yasikusaidie na kukufanya usisamehewe.
Hivyo uwe makini sana wakati wa kuomba msamaha.
5) KUSAMEHE NA KUSAHAU.
Hii hoja imekuwa ikizungumzwa kwa mitazamo tofauti na wataalamu wa kutafsiri neno kusamehe na Kusahau.
Leo naomba tuujue ukweli juu ya neno sahau.
Neno sahau lina maana kutokukumbuka. Sasa suala la kutokukumbuka limejificha kwenye kitu kutojirudia rudia.
Kitu kikijirudia rudia huwa hakisahauriki hata siku moja.
Tambua kuwa mwanadamu Moyo wake umeumbwa kutunza kumbukumbu za mabaya na mazuri, sasa kama mazuri yatamzunguka mwanadamu basi Moyo wake utatawaliwa na kumbukumbu za mazuri, na kama Moyo wake mwanadamu utatawaliwa na mabaya basi utatunza kumbukumbu za mabaya.
Mtu anapokufanyia ubaya, ina maana amekuumiza na kukusababishia kidonda.
Kidonda hicho kitazidi kukuuma endapo hautafanya jitihada za kukitibu, na kinaweza kuwa kikubwa zaidi ikiwa aliyekusababishia kidonda hicho ataamua kukuumiza tena.
Je unatibuje kidonda cha makwazo na mabaya uliyofanyiwa na mtu!? Ni kwa njia ya kumsamehe tu huyo mtu ikiwa amekuomba msamaha au hajakuomba msamaha. Na kidonda hupoa haraka sana ikiwa aliyekusababishia Hicho kidonda atakusaidia kipone kwa kukuomba msamaha.
Ø  Maumivu ya kufanyiwa ubaya na mtu hupona taratibu  ikiwa utaamua kumsamehe huyo mtu. Lakini maumivu hayo hupona haraka sana endapo utaamua kumsamehe huyo mtu na huyo mtu uliye msamehe naye kukuomba msamaha.
Sasa baada ya kupona kwa kidonda cha ubaya uliofanyiwa huwa linabaki KOVU. Kovu ni kumbukumbu ya ubaya ulio wahi kufanyiwa japo haukuumi tena. Je kovu huwa linauma? Kovu huwa haliumi ila ni kumbukumbu ya kidonda kilichowahi kukuuma.
Hivyo kila mtu huwa na makovu ya mambo aliyowahi kufanyiwa, makovu ambayo hawaumi wala hayafanyi uwe na uchungu tena.
Kumbukumbu huwa haifutiki kirahisi hasa mtu mbaya uliyemsamehe akiendelea kukufanyia ubaya, hapo kitakachokuwepo ni kutomlipiza kisasi tu lakini si kwamba hukumbuki.
Naomba niwaulize swali, hivi kama mtu amekuibia mbuzi wako, ukamkamata! Akakuomba msamaha, ukamsamehe. Lakini baada ya mwaka mmoja kupita akaja kukuibia Ng'ombe wako, ukamkamata! Je ukimkamata huwezi ukakumbuka tendo la kukuibia mbuzi alilowahi kukufanyia mwaka ulio pita.? Naamini utakumbuka tu, lakini kukumbuka kwako kuna maana gani? Kuna maana hujamsahau kwa kile alichokutendea. Lakini kukumbuka kwetu sisi hakutufanyi tushindwe kumsamehe au kumuhukumu, na tunaporejea kosa lake la nyuma hakutufanyi tuonekane hatukusamehe. Tutaonekana hatukusamehe ikiwa tukiamua kumuhukumu tutajumulisha adhabu ya kosa la kwanza na kosa hili la sasa, lakini tukimuhukumu kwa kosa la sasa ina maana tulimsamehe kweli kwa kosa la kwanza.
Ø  Kwa kweli watu wamejitahidi sana kuwasamehe wenzao, lakini wamepata taabu sana kusahau ikiwa hao walio wasamehe wameendelea kuwaumiza, kitendo ninachokiita kuyaanika maovu yao yaliyopita kwa wenzao walio wasamehe. Mwaka Jana ulinitukana, nikakusamehe, mwaka huu ukanitukana matusi yaleyale eti ufikiri nilisahau hivyo siwezi kukumbuka, ni kweli kabla hujarudia kunitukana nilikuwa nimesahau, lakini uliponitukana tena ina maana umeamua kunikumbusha, na hivyo utanifanya nionekane kama huwa sisahau na hivyo huwa sisamehi. Ki ukweli hapa kilichopo ni sisi tulio okoka kuwa wavumilivu tu na kutokulipiza kisasi, na tusiruhusu ubaya watu wanaotufanyia utufanye nasi tuwe wabayam
Unakumbuka wana wa Israeli? Shetani alizidi kuwakumbusha kule Misri, na walikumbuka kweli, lakini walizidi kusonga mbele.
Ø  Na sisi watu wakitufanyia ubaya, tukiwasamehe, Shetani atawatumia tena kutufanyia ubaya ili tukumbuke ubaya wao na hivyo kuwa na uchungu zaidi kiasi cha kutowasamehe tena. Lakini Shetani hata akitukumbusha hatuna budi kusimamia msimamo wetu wa kusamehe tu! Hatuwezi kusema tutasahau ubaya wa watu na kuupuuza ili tuonekane wajinga, hapana ubaya hukumbushwa kwa ubaya lakini huondolewa kwa wema"Msamaha"
Na mazuri hukumbushwa kwa mazuri, na huondolewa kwa mabaya. Hivyo tusikubali ubaya ukaondoa mazuri, au ubaya ukazidi kuzalisha ubaya. Msamaha ni dawa ya kuuondoa ubaya na kuendeleza mazuri

6)KUSAMEHE HAKUMAANISHI MAMBO YAFUATAYO:-
Biblia inasema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. Hosea 4:6.
Sisi hatuwezi tukawa wajinga kwa kulitumua neno la Samehe Saba mara Sabini, kuendelea kufanyiwa mabaya kila wakati na watu walewale huku wakituomba msamaha na kusema imeandikwa "Samehe saba mara sabini"
Unajua hili neno lina maanisha nini? Mtu huyo akufanyie kosa hilo hilo kwa siku hiyo hiyo na kila akifanya kosa hilo kwako akija kukuomba msamaha msamehe hata mara sabini hii ilimlenga mtu yule ambaye amekuwa akitenda dhambi au makosa pasipo kukusudia yaani anatenda kwa bahati mbaya tu. Sasa Wewe nifanyie makosa au nitendee dhambi kwa makusudi ufikirie nitakusamehe!
Hapa wa kuwafundisha si watu wanaotakiwa kutoa msamaha tu na kusahau, lakini hata watenda makosa au dhambi wanatakiwa wafundishwe kutotenda makosa au dhambi kwa kujua wanayo fulsa ya kuomba msamaha. Kuna makosa au dhambi za makusudi hakika hizo usiposamehewa usimlaumu mtu.
Hivyo kusamehe hakumaanishi mambo yafuatayo:-

A) Kumsamehe mtu makosa yake hakumaanishi umepuuzia makosa yake.
Tukipuuza hayo makosa itamaanisha tunakubaliana nayo na hayana madhara. Biblia inatuonya tusifanye hivyo:-
Isaya 5:20  "Ole wao wasemao Uovu ni wema, na kwamba wema ni Uovu, watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza, watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu".
B) Kumsamehe mtu makosa yake haimaanishi kumbukumbu hiyo hawezi kukumbukwa.
Mfano Mfalme Daudi licha ya kusamehewa dhambi zake, lakini ziliandikwa na kuwa kumbukumbu mpaka leo.
2Samweli 12:9-13

C) Haina maana kumsamehe mtu basi ni kumpa nafasi ya kuendelea kukufanyia ubaya.
Kwa mfano;- Umemkopesha mtu pesa akidai anataka kumuuguzia mgonjwa, lakini akatumia kunywea pombe! Akashindwa kukulipa, na akaomba umsamehe hilo deni , na kweli akamsamehe. Lakini akaja siku nyingine kukukopa pesa, hapo unaweza usimpe hata kama unazo na usiwe umetenda dhambi yoyote.
Maandiko ya kujifunza ni:- Zaburi 37:21, Mithali 14:15, Mithali 22:3, Wagalatia 6:7.
Zaburi 37:21 "Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukalimu."
Wagalatia 6:7 "Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi ; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna."

D) Haina maana kufundishwa kusamehe basi mtu akiwa anakufanyia mabaya kwa makusudi basi utakuwa unamsamehe tu.
Hata Mungu hawezi msamehe mtu anayefanya dhambi kwa kudhamilia au kukomoa.
Methali 28:13, Matendo 26:20, Waebrania 10:26 "Maana kama tukifanya dhambi kusudi, baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, habaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi".
Pia unaweza kusoma Zaburi 139:21-22.
Hakika mtu ambaye yeye hawasamehi wenzake, akikukosea na kuja kuomba msamaha kwako unaweza usimsamehe kwani hayo ni malipo yake!
E) Kuna makosa ya kuhisi. Makosa hayo hayafai kutusumbua na kama kuna msamaha wa kutoa ni budi kuutafuta kwanza ukweli. Hakika ukweli utakufanya utoe msamaha kwa amani. Utajisikiaje ukitoa msamaha kwa kosa la kuhisi ukidhani ni kosa Dogo kisha ukaja kugundua ni kosa kubwa?
Hakika ni bora kuchunguza kosa kabla ya kulitolea msamaha.

MUNGU AKUBARIKI SANA

Maoni

  1. Asante nimejifunza kitu hapa

    JibuFuta
  2. Mungu awa zidishie ni Mtumishi Chris kutoka true way deliverance ministry .Mombasa Shanzu
    .Pendua

    JibuFuta
  3. mafundisho haya ni mazuri nimeyapenda na yamenisaidia kuachilia msamaha na kusahau

    JibuFuta
  4. Barikiwa sana kwa somo hili ni jana tu usiku nimefanya maamuzi ya kumsamehe mtu jambo kubwa sana ambalo sikutegemea kusamehe na wala hakuomba msamaha

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FAIDA YA KUJAA ROHO MTAKATIFU

🔰 MBINU ZA KUFUNGA NA KUOMBA 🛐*